Sunday, April 21

AUBA-MABAO Akiongezewa Ozil mwingine, Arsenal kila siku sherehe

0


LONDON, England

KAMA umesahau kitendo cha Arsenal kumsajili
Pierre-Emerick Aubameyang kwa kitita cha pauni milioni 60 mwaka jana, ndicho
kilichopunguza mawazo na huzuni na kuamsha mwanga wa matumaini miongoni mwa
mashabiki wengi wa klabu hiyo.

Arsenal ilifanikiwa kumnasa mpachika mabao huyo
katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili wa mwezi kama huu, kazi kubwa
ikifanywa na Arsene Wenger.

Kocha huyo wa zamani wa Arsenal, alijikuta kwenye wakati
mgumu kusaka mfungaji mzuri wa mabao hasa baada ya kuondokewa na nyota watatu; Olivier
Giroud, Theo Walcott na Alexis Sanchez.

Baada ya kufanikiwa kumpata Aubameyang, nyota huyo
amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuibeba timu hiyo, licha ya kwamba kwa namna moja
au nyingine umuhimu wake hauzungumzwi sana.

Tangu afunge bao lake la kwanza katika mechi ya
kwanza kuitumikia Arsenal, mnamo dakika ya 37 ya mchezo wao dhidi ya Everton, Aubameyang
ameshafunga jumla ya mabao 24 kwenye mechi 34 za Ligi Kuu England.

Kwenye takwimu hiyo, Mgabon huyo amepitwa na nyota
wa Liverpool, Mohamed Salah tu ambaye amefunga mabao 27.

Zaidi ya hapo, kwenye zile ligi tano kubwa za Ulaya,
wachezaji pekee waliomzidi Aubameyang kwa jumla ya mabao ni Cristiano Ronaldo
(32) na Lionel Messi (30).

Umuhimu huo mkubwa wa Aubameyang umekuja katika
nyakati ambazo Arsenal ina uhaba wa wachezaji wabunifu ambao kazi yao ya
kutengeneza nafasi za mabao ingemalizwa vizuri na straika huyo.

Ikumbukwe miaka iliyopita, mashabiki wa Arsenal walikuwa
wanalilia klabu yao isajili mpachika mabao hodari wa kumalizia kazi za akina Cesc
Fabregas, Samir Nasri na Andrey Arshavin, lakini kwa sasa wote hawapo.

Mchezaji pekee wa Arsenal mwenye uwezo mkubwa wa
kutengeneza nafasi za mabao ni Mesut Ozil ambaye hata hivyo, ameanza mechi
mbili tu za Ligi tangu katikati mwa Novemba mwaka jana.

Mwingine ni Aaron Ramsey ambaye amebakiza miezi michache
kabla ya kuondoka Arsenal kujiunga na Juventus ya Italia, hivyo kuacha majukumu
kwa Alex Iwobi.

Lakini cha ajabu, mpaka sasa Iwobi hajaweza kutoa pasi
ya bao hata moja ambalo limefungwa na Aubameyang kwenye Ligi Kuu England.

Pia, unaweza ukashangaa kusikia hili, lakini takwimu
zinaeleza kwamba Aubameyang alipokuwa Dortmund aliweza kutoa pasi 20 za mabao
katika mechi 134 za Bundesliga na tangu atue Arsenal, jukumu hilo limehamia
kwake.

Aidha, takwimu zinasema kwamba Salah ndiye mshambuliaji
pekee mwenye pasi nyingi za mabao kuliko Aubameyang, tangu nyota huyo acheze
mechi yake ya kwanza Arsenal.

Kama hiyo haitoshi, Aubameyang ameshajiweka kileleni
kama straika mwenye mabao na asisti nyingi Ligi Kuu England kuliko Harry Kane na
Sergio Aguero, tangu alipotua Arsenal.

Hoja ya umuhimu wake Arsenal inatetewa zaidi na
takwimu yake kuwa, mabao 24 aliyoifungia Arsenal yamechangia pointi 16 kwenye
Ligi Kuu, wakati huo huo mabao 26 ya Salah yamechangia pointi nane tu kwa
Liverpool.

Katika msimu huu tu, hakuna mchezaji aliyefunga
mabao yenye thamani zaidi kwa timu yake kama Aubameyang.

Kichapo cha bao 1-0 walichopata Arsenal wikiendi iliyopita
dhidi ya West Ham, kilimnyima Aubameyang nafasi ya kuwa mchezaji wa tano kufikisha
mabao 25 kwenye Ligi Kuu England haraka zaidi.

Aidha, kama angefunga bao dhidi ya wagonga nyundo
hao wa London, angekuwa mchezaji wa pili asiye Mwingereza kufikisha idadi hiyo baada
ya straika wa zamani wa Liverpool, Fernando Torres.

Kumsajili Aubameyang ilikuwa ni jambo zuri zaidi
kuwahi kufanywa na Wenger licha ya kutengeneza utamaduni wa kuthamini vipaji
vya wachezaji wadogo tangu alipohamia kwenye Uwanja wa Emirates na timu yake
hiyo mwaka 2006.

Mara ya mwisho kwa Wenger kusajili straika mwenye
umri mkubwa ilikuwa ni mwaka 1999, walipomnyakua Davor Suker.

Na Aubameyang alitua Arsenal akiwa na umri wa miaka 28,
unaweza kusema kuwa Wenger alishindwa kupingana na ukweli kwamba licha ya
straika huyo kuwa na umri mkubwa, lakini ubora wake ulijulikana wazi.

Juni mwaka huu Aubameyang atafikisha miaka 30. Umri
ambao Wenger alikuwa akiuza wachezaji. Lakini Emery, atamfaidi straika huyo
zaidi na zaidi. Ni suala la kumwongezea wachezaji wa kumlisha nafasi za mabao.

Share.

About Author

Leave A Reply