Wednesday, August 21

…Ataja first eleven yake

0


ZAITUNI KIBWANA

KATIKA kuonyesha jinsi alivyo makini, Kocha Mkuu wa Yanga,
Mwinyi Zahera, ametaja kikosi chake bora cha Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu,
huku akiwajumuisha wawili tu kutoka katika timu yake.

Ligi hiyo inafika tamati leo, huku Simba wakiwa ndio
mabingwa wapya wa 2018/19, wakifanikiwa kutetea taji lao walilolitwaa msimu
uliopita, wakati Yanga ikiambulia nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 86 dhidi
ya 92 za Wekundu wa Msimbazi kabla ya mechi yao ya leo.

Akizungumza na BINGWA jana baada ya mazoezi ya timu yake
kujiandaa na mchezo wa mwisho dhidi ya Azam FC utakaopigwa leo Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam, Zahera, alisema amejipanga kushambulia mwanzo mwisho.

“Sina ninachopata katika mechi hii ambayo ni ya
mwisho, hivyo nitashambulia mwanzo mwisho ili kuwavuruga Azam na nipate bao la
mapema tu,” alisema.

Juu ya kikosi chake cha msimu, kocha huyo alisema
amechagua wachezaji bila kujali timu zao zaidi ya ubora wao waliouonyesha msimu
mzima.

Aliwataja wachezaji hao kuwa kipa ni wa Mbao FC,
Metacha Mnata, Aron Lurambo (KMC), Ally Mtoni ‘Sonso’ (Lipuli), Kelvin Yondani (Yanga),
Mudathiri Yahaya (Azam), Clatous Chama (Simba), Jonas Mkude (Simba), Emmanuel
Okwi (Simba), Meddie Kagere (Simba), Heritier Makambo (Yanga) na Ramadhani
Singano ‘Messi’ (Azam).

Alisema kati ya wachezaji hao, watakaobadilika ni
Chama ambaye atampisha Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Yanga na Mkude
atakayebadilishana na Papy Tshishimbi (Yanga).

“Golini ni Mnata, nadhani amecheza vizuri sana, beki
wa kulia Lurambo, mabeki wa katikati ni Yondani na Sonso, hawa wamefanya vema.

“Viungo ni Mudathir, Singano na Mkude, winga wa
kushoto ni Emmanuel Okwi, kiungo wa mbele ni Chama na washambuliaji wawili ni Kagere
na Makambo,” alisema.

Alisema msimu huu kulikuwa na matukio mengi ya
kusisimua lakini jambo ambalo hawezi kulisahau ni changamoto ya waamuzi.

“Waamuzi wamekuwa changamoto sana msimu huu, siwezi
kuwasahau kwa sababu wao ndio walikataa bao dhidi ya Mtibwa, leo hii labda
tungekuwa tunaongea mengine,” alisema.

Yanga inawakaribisha Azam huku ikiwakosa wachezaji
wake sita wanaokabiliwa na majeraha ambao ni Juma Abdul, Andrew Vincent
‘Dante’, Ibrahim Ajib, Paul Godfrey ‘Boxer’, Haruna Moshi ‘Boban’ na Mohammed
Issa ‘Mo Banka’.

Share.

About Author

Leave A Reply