Tuesday, August 20

Simba waitikisa Mara

0


NA MAREGESI NYAMAKA, MUSOMA

MABINGWA
watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, jana walipokewa na umati mkubwa wa
mashabiki wa timu hiyo walipokuwa wakiingia Mara, mjini Musoma kwa ajili ya
mchezo wao wa leo dhidi ya Biashara United.

Umati
huo wa mashabiki ulianza kujitokeza kwa wingi zaidi Bunda Mjini ambapo walijipanga
barabarani wakidai wanasubiri timu hiyo tangu saa 12:00 asubuhi.

“Tupo
hapa tangu saa 12:00 alfajiri kwa kuwa ni muda mrefu hatujaiona timu yetu,”
alisema Ally Juma ambaye alilalamikia kitendo cha gari iliyoibeba timu hiyo
kushindwa kusimama kwa ajili yao.

Gari
hiyo aina ya Toyota Coaster yenye namba T457 DPU iliyobeba kikosi hicho cha
Simba, ilipita eneo hilo la Bunda saa 5:00 asubuhi.

Shangwe
hilo la mashabiki liliendelea hadi kwa mashabiki wengine wa Musoma ambapo ndipo
utakapochezwa mtanange huo kwenye Uwanja wa Karume, msafara huo uliongozwa na
pikipiki na gari la polisi kwa ajili ya usalama barabarani.

Simba
watakutana na Biashara United leo baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya
KMC ya Kinondoni kwenye mchezo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Wekundu
hao wa Msimbazi watashuka dimbani wakiwa wanahitaji kuendeleza wimbi la ushindi
ili waendelee kujiwekea matumaini ya kutetea ubingwa wao msimu huu.

Simba
wako kwenye harakati za kuhakikisha wanatetea ubingwa huo wa Ligi Kuu ili
warejee tena kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutolewa hatua
ya robo fainali na TP Mazembe.

Simba
wamekuwa kwenye kazi nzito ya kucheza viporo vyao kila baada ya siku moja tangu
walipotolewa ili waweze kulingana na wengine ambao tayari wamekwishafikisha
mechi 32 na wao wakitarajiwa kucheza mechi ya 27 leo.

Kwa
sasa Simba ambayo imecheza michezo 26 inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi
66, wakiwa nyuma ya mahasimu wao Yanga wenye pointi 74 baada ya kucheza michezo
32.

Lakini
Simba watakuwa na kazi ngumu kwa Biashara United ambao wako nafasi ya 19 baada
ya kucheza mechi 34, kutokana na kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Share.

About Author

Leave A Reply