Wednesday, August 21

Simba kuiteka Moro

0


WINFRIDA MTOI

WANACHAMA na mashabiki wa Simba kutoka maeneo
mbalimbali, wameanza kumiminika mjini Morogoro, tayari kulipokea kombe lao la
ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watakalokabidhiwa baada ya mchezo dhidi ya
Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Mchezo huo ni miongoni mwa 10 zitakazochezwa kwenye
viwanja mbalimbali nchini kuhitimisha msimu huu wa 2018/19, huku tayari bingwa
akiwa ameshapatikana ambaye ni Simba.

Simba waliomba kukabidhiwa kombe lao juzi Jumamosi
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, walipovaana na Biashara United, lakini
ilishindikana kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF).

Akizungumza na BINGWA jana kwa simu kutoka Morogoro,
Katibu wa Matawi ya Simba, mkoani humo, Mkombozi Mruma, alisema wameandaa
sherehe ‘bab kubwa’ itakayofanyika katika tawi la Shujaa.

Mruma alisema sherehe hiyo, itafanyika baada ya mchezo
huo, itakayokwenda sambamba na futari ya pamoja na wachezaji, viongozi wa klabu
na wanachama wa Simba wa Morogoro na mikoa mingineyo watakayojitokeza.

Alisema wanafanya hivyo kwa sababu ni mara ya kwanza
kwa timu hiyo kukabidhiwa kombe la ubingwa katika ardhi ya Morogoro.

“Ilikuwa ni kilio chetu cha muda mrefu kuona siku
moja Simba inakabidhiwa ubingwa Morogoro, Mungu amejibu maombi yetu na sisi
lazima tufanye kitu cha ukumbusho,” alisema Mruma.

Akiuzungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba,
Patrick Aussems, alisema: “Japo tumeshatwaa ubingwa, lakini tutacheza kama
kawaida yetu ili tuweze kumaliza ligi kwa heshima, hivyo wapinzani wetu
wajiandae kufungwa.”

Tayari mashabiki wa Simba wameanza kufurika mjini
Morogoro ambapo baada ya mchezo huo, sherehe zitaanzia uwanjani hapo na
kuendelea katika maeneo mbalimbali ya starehe na kwingineko.

Share.

About Author

Leave A Reply