Sunday, August 18

Sevilla wathibitisha safari ya Tanzania

0


MWANDISHI WETU

MABINGWA mara tano wa michuano ya UEFA Europa
League, Sevilla, wamethibitisha kuja nchini kuvaana na timu ya Simba au Yanga.

Safari ya klabu ya Sevilla ambayo inashiriki Ligi
Kuu Hispania maarufu La Liga, imewezeshwa na Kampuni ya michezo ya kubahatisha
SportPesa.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya La Liga Kimataifa, Oscar
Mayo, alisema mradi wa La Liga World Challenge unakusudia kupanua brandi ya La
Liga duniani.

“Ni nafasi adimu kwa kila mtu kwamba mashabiki
wetu Tanzania wataiona klabu maarufu ya Sevilla,” alisema.

Sevilla maarufu kama Nervionenses, watacheza na timu
moja washirika wa SportPesa kati ya Simba au Yanga Mei 23 mwaka huu, katika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa,
Tarimba Abbas, alisema wanafanya kazi na baadhi ya taasisi kubwa za soka
duniani, hivyo kuna umuhimu wa kuleta nchini uzoefu wao.

“Ushirikiano huu unatufanya tuone umuhimu wa kuleta
uzoefu wao nchini ili kuwapa nafasi Watanzania kuifurahia Sevilla ambayo ni
moja ya timu kubwa Ulaya,” alisema Tarimba.

Sevilla inakuwa timu ya pili kuletwa nchini na
SportPesa baada ya Everton ya England iliyokuja miaka miwili iliyopita.

Mabingwa hawa mara moja wa La Liga, wanarudi Afrika
kabla hata ya kumaliza mwaka tangu kucheza Spanish Supercup jijini Tangiers,
Morocco.

Aidha, walicheza Morocco miaka minne iliyopita dhidi
ya Hassania Union Sport d’Agadir.

Naye Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Wilfred Kidao, alisema si jambo dogo kupata ugeni wa Sevilla ambayo inashiriki
ligi bora.

“Sevilla ina wachezaji 11 wanaocheza timu za taifa
kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Argentina, Hispania na Italia, hivyo kama TFF
tunaahidi kushirikiana na SportPesa kuhakikisha maandalizi yote yanakwenda
vizuri kuelekea mchezo huo,” alisema Kidao.

Share.

About Author

Leave A Reply