Tuesday, August 20

Salamba apata shavu Ureno

0


WINFRIDA MTOI

UONGOZI wa klabu ya Simba umepanga kuwatoa kwa mkopo
nyota wake watatu akiwamo mshambuliaji, Adam Salamba, anayekwenda kukipiga
nchini Ureno.

Salamba ambaye alisajiliwa na Simba msimu huu
akitokea Lipuli FC kwa dau la Sh milioni 40, amekosa namba ya kudumu katika
kikosi hicho cha Msimbazi kinachonolewa na kocha, Patrick Aussems, kutokana na
kushindwa kumudu ushindani uliopo.

Uwepo wa washambuliaji hatari kikosini hapo kama
vile Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi, ulikuwa ni sababu tosha kwa
Salamba kushindwa kutamba ndani ya Wekundu hao wa Msimbazi.

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba,
kimelipasha BINGWA kuwa wachezaji wengine ambao wanatarajiwa kutolewa kwa mkopo
baada ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kumalizika ni Rashid Mohammed,
anayekwenda nchini Kenya na Abdul Mohammed, ambaye haijajulikana atakwenda timu
gani.

Aidha, chanzo hicho kilieleza kwamba, tayari Aussems
amekabidhi ripoti yake kwa uongozi inayoonyesha wachezaji watakaoachwa lakini hakuwataja
kwa majina.

Hata hivyo, mtoa taarifa huyo alisema alichoeleza
kocha ni kwamba wataachwa  wachezaji
wanne wa kigeni na watatu wazawa.

“Ripoti ya kocha haijawataja kwa majina wachezaji
ambao wataachwa msimu huu lakini idadi yao ni saba, ila katika orodha hiyo
sidhani kama Zana (Coulibally) atakosekana,” kilisema chanzo hicho.

Katika hatua nyingine, chanzo hicho kilieleza kwamba
kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mohammed Ibrahim ‘Mo’, pia anajadiliwa ili
kujiridhisha kama anaweza kubaki kikosini msimu ujao.

“Kimsingi kikosi cha Simba hakitabadilika sana maana
tayari tumemwongezea Bocco mkataba, kuhusu wachezaji wapya bado tunazungumza
nao ila siwezi kuwaweka wazi,” kilieleza chanzo hicho.

Share.

About Author

Leave A Reply