Friday, April 19

Mwanamke hapaswi kufanyiwa hivi kama unahitaji amani

0


NA RAMADHANI MASENGA

MWANAMKE ni binadamu kama mwanaume, anahitaji amani, furaha, kupewa thamani na kuheshimiwa kama anavyohitaji mwanaume.

Kosa kubwa wanalofanya wanaume wengi
katika mahusiano ni kuwafanya wanawake wao kukosa uhuru na thamani.

Unakuta kama ni pesa ya matumizi,
mume anampa mke kiwango kile kile anachopaswa bila kuzidisha kiwango chochote.

Wanawake wengi katika baadhi ya
mahusiano wanaishi maisha yasio na tofauti na watoto wadogo kwa wazazi wao.

Kila kitu ni lazima waombe, kila
jambo ni lazima wawasikilize wenzao wanataka nini, lakini wao hawana uhuru wa
kusikilizwa ama kufanyiwa jambo wanalotamani kufanyiwa.

Wanaume wengi huona hali hii kama ya
 kawaida ila ukweli ni kwamba ni
hatari  inayoua upendo na hamasa ya wanawake kwa waume zao.

Mwanamke ni mshirika kwa mwanaume, kitendo
cha mwanaume kuanzisha uhusiano naye wa kimapenzi maana yake anataka kumfanya
mwanamke husika kuwa sehemu yake.

Sasa kama kweli ni sehemu yako,
sehemu muhimu ya maisha yako, kwanini humpi hadhi inayostahili?

Wapo baadhi ya wanaume hawajulikani
kwa wake zao wakiwa na pesa wala kipindi hawana, siku zote wao ni hali mbaya tu
kwa wake zao, hii ni hatari mno.

Ifahamike, hakuna binadamu
asiyependa kuishi vizuri ama kupata vizuri, sasa unavyomnyima fursa menzako kuonja
ladha ya mafanikio ama chochote cha maana kutoka kwako, unamuumiza na kumfanya
asione thamani yake kupitia wewe.

Mke wako anahitaji umiliki, awe na
furaha na ajiachie kwa kuwa na wewe, hivyo unavyomfanya asijione sehemu muhimu
ya maisha yako si tu unamnyima furaha, ila pia unaufanya uhusiano wako uwe
dhaifu.

Kama mke wako haoni raha na amani
kutokana na mtindo wa maisha yenu, unadhani hali hiyo ataendelea kuwa nayo
mpaka lini?

Kama binadamu ni lazima atamani
maisha ya kujiachia na kuiona thamani na hadhi yake stahili, hivyo kuwa makini,
ukiacha kuziba ufa utajenga ukuta.

Mke wako ni zaidi ya rafiki, ni
mshirika wako wa kihisia, mwili na maisha, mtu wa namna hii hapaswi wala
kustahili kuonwa wa kawaida.

Mpe uhuru fulani katika matumizi na
maisha yenu, mfanye ajione yuko kwake si yuko kwako.

Baadhi ya wanawake wanafanya mambo
yasiyostahili katika maisha yao, mbali na mambo mengine ila tabia ya waume zao
kuwaona ama kuwatendea kama watoto wadogo ni sababu nyingine.

Mwanaume anaenda kwenye matembezi na
‘pocket money’ ya kutosha ila mkewe anamuacha na pesa kamili ya matumizi
muhimu.

Hata akitamani soda ama kitu kingine
hawezi kununua, hii si sawa na haistahili kuwa hivi.

Kumnyima uhuru na hadhi anayostahili
kunamfanya mwanamke husika ajione yupo kifungoni badala ya kuwa katika
uhusiano.

Ndio maana tafiti zinaonesha katika
ndoa nyingi wanawake hawana furaha bila sababu ya kueleweka.

Wanawake wengi hawana furaha na
waume zao hawajui ni kwanini, hata wakati mwingine wanawake wenyewe wanasahau
kwanini hawana furaha.

Ila ukichunguza kwa makini kwa jicho
thabiti la kitaalamu, unagundua wengi wao hawana furaha katika mahusiano yao
kutokana na namna wanavyofanywa kuishi.

Wakati baadhi ya wanawake wakiona
waume zao wanafanikiwa hupata furaha isiyo kifani, wapo wengine ambao wanaona ni
kawaida tu.

Hawana furaha kwa sababu wao huwa
hawaoni tofauti kati ya waume zao wakiwa na fedha na kipindi wakiwa
hawana.

Wao kila siku hali ni mbaya tu yaani
wakati wote ni kuvumilia, wanaume inabidi kubadilika.

Toka na mkeo ‘outing’, mpatie pesa
zisizo katika matumizi sahihi na mwambie atumie anachopenda yeye kutumia.

Mpe uhuru ili akuthamini zaidi, mthamini
ili akujali na kukusikiliza zaidi, mapenzi ni urafiki wa ndani wa hisia, miili
na fikra, mjali mwenzako aone hali hii kupitia matendo na kauli zako.

Katika maisha kila siku ni kupambana
na changamoto, ila hali hii isikufanye umnyime mwenzako fursa ya kufurahi na
kujidai na maisha yake.

Mwenzako anapaswa kusisimuliwa na
matendo na kauli zako, namna unavyowatendea watoto wako haipaswi kuwa sawa na
unavyomtendea mkeo.

Mkeo ni sehemu yako, kama ambavyo
unavyopaswa kuheshimiwa, kujaliwa na kusikilizwa.

Mkeo pia anahitaji nafasi hiyo maana
naye ni binadamu kamili kama wewe na si nusu yake.

Share.

About Author

Leave A Reply