Tuesday, August 20

Kaseja: Msimbazi hawana jipya

0


NA ZAITUNI KIBWANA

KIPA mkongwe katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Juma
Kaseja, amesema hatishwi na safu ya ushambuliaji ya timu ya Simba inayoongozwa
na Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco.

Kauli hiyo ya Kaseja inakuja siku chache kabla ya
timu yake ya KMC kuvaana na Wekundu hao wa Msimbazi katika mchezo unaotarajiwa
kupigwa Ijumaa wiki hii kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

KMC ambao ni wenyeji wa mchezo huo, wanashika nafasi
ya saba kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kujikusanyia pointi 42 wakicheza
mechi 32.

Msimu uliopita Kaseja aliwashangaza  Simba kwa kutibua rekodi yao ya kutofungwa
Ligi Kuu, baada ya kuokoa mkwaju wa penalti huku timu yake ya Kagera Sugar
ikiibuka na ushindi wa bao 1-0. 

Akizungumza na BINGWA jana, Kaseja alisema wachezaji
wanaocheza Simba ni wale wale wa siku zote hivyo hakuna kitu kipya ndani ya
kikosi hicho.

“Hakuna mchezaji ambaye tunamhofia katika kikosi cha
Simba kwa sababu wachezaji wote tunawafahamu na hakuna mgeni wa kututisha,”
alisema Kaseja.

Akizungumzai maandalizi yao kuelekea  mtanange huo, Kaseja alisema kocha wao mkuu,
Etienne Ndayiragije, anaendelea kuangalia mapungufu ya kikosi ili ayafanyie
kazi kabla ya mechi.

“Maandalizi yamekamilika na sasa mwalimu anaangalia
mapungufu yaliyopo yafanyiwe kazi, yale mazuri tutayaendeleza ili tupate
uhakika wa kuvuna pointi tatu,” alieleza Kaseja.

Kwa upande wake, Ndayiragije, alisema hawana presha
na mchezo huo bali wanasubiri kuwakabili wapinzani wao hao.

“Tutapambana ili tupate pointi tatu muhimu na
kusogea nafasi za juu kwenye msimamo, kwetu kila mchezo tunaupa kipaumbele
hatudharau timu yoyote,” alisema Ndayiragije.

Share.

About Author

Leave A Reply