Friday, August 23

Kama unaishangaa Serengeti Boys huwezi kuzipongeza Simba, Stars

0


NA HASSAN DAUDI

USHINDI wa mechi mbili tu ungetosha kuipeleka
Tanzania katika fainali za Kombe la Dunia za vijana wenye umri chini ya miaka
17 zitakazofanyika mwaka huu nchini Brazil.

Kuiweka vizuri, ndani ya mwaka mmoja, historia tatu
zingekuwa zimeandikwa kwani tayari Simba na Stars zilishachukua nafasi. Wekundu
wa Msimbazi walitinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya
kwanza tangu mwaka 1994.

Stars nayo ilikata tiketi ya kushiriki fainali za
Afcon za mwaka huu kule Misri. Kabla ya hilo kutimia mwezi uliopita, mashabiki
wa kandanda nchini waliishia kuitazama michuano hiyo kupitia runinga tangu
mwaka 1980.

Serengeti ilishindwa kuungana na Simba na Stars
kuendeleza ndoto ya wadau wa kandanda la Tanzania, baada ya kupoteza mechi zote
tatu za Kundi A la fainali za Afcon kwa vijana wenye umri huo, michuano ambayo
ndiyo inayotoa nafasi nne za kwenda Brazil.

Huku hilo likishindikana, binafsi ningependa kuibuka
na hoja tofauti kidogo ambayo msingi wake ni shutuma alizoelekezewa kocha wa
Serengeti Boys, Oscar Mirambo, wakati michuano hiyo ya wiki mbili ikiendelea
katika viwanja vya Taifa na Chamazi jijini Dar es Salaam.

Nikiri kuwa huenda kocha Mirambo ameponzwa na
saikolojia ya mashabiki wa vijana wake. Isingekuwa rahisi kuwaaminisha
Watanzania kuwa wanaikosa nafasi ya kwenda Kombe la Dunia kwa kukosa ushindi wa
mechi mbili tu.

Kwa namna morali ilivyokuwa juu kabla ya mashindano,
Mirambo na wasaidizi wake wa benchi la ufundi wanapaswa kukubali tu kwamba
saikolojia ya wengi ilishatangulia Brazil, wakiamini hakuna cha kuizuia kwa
kuwa ilikuwa katika ardhi ya nyumbani.

Kama ilivyo kwa mashabiki wote duniani, ingehitaji kazi
kubwa kuwaaminisha Serengeti Boys haitakwenda na imeyaaga mashindano ya Afcon
U-17, ikiwa imefungwa jumla ya mabao 12 katika mechi tatu dhidi ya Nigeria,
Uganda na Angola.

Nikirejea katika hoja yangu, nianze kwa
kutokubaliana na madai ya uenyeji kuwa ilikuwa sababu ya msingi kwa Serengeti
Boys kuipeleka Tanzania. Licha ya kwamba ni dhana iliyozoeleka, soka la kisasa
haliipi nafasi kubwa mbele ya ubora wa timu husika.

Bahati mbaya, hata historia ya michuano yenyewe
haioneshi kuwa Serengeti Boys ilikuwa na nafasi ya ubingwa kwa kuwa ilikuwa
nyumbani. Tangu mwaka 1995, ni Gambia pekee iliyoweza kuziandaa na kutwaa
ubingwa wa fainali hizo. Pia, mwaka jana zilifanyika Gabon lakini Mali ndiyo
iliyoibuka kidedea.

Katika kile nilichokiona, hakuna namna ya kuepuka
ukweli kwamba kuvurunda kwa Serengeti Boys ni sehemu ndogo tu ya udhaifu mkubwa
wa soka la vijana nchini, hivyo kuibua hofu juu ya njia iliyotumika kuzivusha
Simba na Stars.

Wataalamu wa soka wanaweza kukubaliana na hoja yangu
kwamba, ili kujijengea misingi imara katika ramani ya mchezo huo ulimwenguni,
mafanikio ya timu ya taifa yanatakiwa kuakisiwa na hatua za chini (timu za
vijana).

Nikizitolea mfano Hispania, mafanikio ya timu yao ya
taifa yanaakisiwa na kile kinachofanywa na vijana wao wa chini ya umri wa miaka
17 ambao mwaka juzi walifika fainali ya Kombe la Dunia. Iko hivyo England, Ujerumani,
Brazil na katika mataifa mengine yanayosifika kwa maendeleo ya kandanda.

Ingekuwa hivyo kwa Tanzania, basi timu nyingine saba
zilizocheza Afcon U-17 pale Taifa na Chamazi zingeihofia Serengeti Boys hata
kabla ya kutua nchini, zikitambua kuwa inatokea iliko Simba na Stars zilizotikisa
Afrika mwaka huu.

Zaidi ya hapo, ni bahati na ujanjaujanja tu.

Share.

About Author

Leave A Reply