Tuesday, August 20

Hesabu zimetiki Yanga

0


TIMA SIKILO                          

HATIMAYE Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amehakikishiwa
kusajili wachezaji sita wa nguvu wa kimataifa watakaokifanya kikosi chake kuwa
tishio katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Msimu huu haukuwa mzuri kwa timu hiyo kutokana na
kushindwa kusajili wachezaji wa kiwango cha juu, hali iliyosababisha mashabiki
wao wasiwe na matumaini ya kutwaa ubingwa na hata kufanya vizuri kimataifa.

Hata hivyo, mara baada ya msimu kuanza kikosi cha Zahera
kilifanya vizuri katika mechi za mwanzo na kujikuta kikiongoza ligi kwa muda
mrefu kabla ya kupoteza mwelekeo kwenye mechi za hivi karibuni walipokubali
vipigo ama kutoa sare.

Japo Yanga inaongoza ligi kwa sasa ikiwa imekusanya pointi
74, lakini matumaini ya kutwaa ubingwa yanaonekana kufifia.

Hilo linatokana na ukweli kwamba Simba waliocheza
mechi chache wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa iwapo watashinda mechi zao 10
zijazo, kwani watakuwa wamewapita pointi wapinzani wao hao.

Kwa kufahamu hilo, mabosi, matajiri wa Yanga na
mashabiki, wameamua kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao wakipania kusajili
wachezaji wa kiwango cha juu hasa kutoka nje ya Tanzania.

Tayari kocha wa Wanajangwani hao, Zahera, ameweka
wazi kitita cha fedha  anazohitaji ili
kumwezesha kusajili wachezaji anaowataka kikosini.

Katika mahojiano na BINGWA, Zahera alisema anahitaji
kitita cha Dola za Marekani 300,000 (sawa na Sh milioni 689) kusajili wachezaji
watakaokuwa tishio na kumaliza kabisa ubabe wa wapinzani wake.

“Nina imani katika kiasi hicho siwezi kukosa
wachezaji kumi wa Dola za Marekani 30,000 (sawa na Sh milioni 70) ambao
wataifanya Yanga kuwa tishio msimu ujao,” alisema Zahera.

Kutokana na ombi hilo la Zahera, Mwenyekiti wa Yanga
bungeni, Anthony Mavunde, amesema kwamba tayari wameshapata fedha za kuwawezesha
kusajili wachezaji zaidi ya sita wenye kiwango cha kimataifa.

Alisema fedha hizo walizozipata kupitia michango ya
wabunge na wadau wengine nchini, zinaweza kuongezeka na hivyo kusajili
wachezaji wengi zaidi wenye kiwango cha juu.

“Tunawaomba wote wanaoitakia mema Yanga wajitokeze
kuichangia timu yao ili uongozi mpya utakapopatikana uweze kushirikiana na
mwalimu wetu Zahera kusajili wachezaji watakaoifanya Yanga kuwa moto msimu
ujao,” alisema Mavunde.

Hadi sasa Wanajangwani hao wamecheza michezo 32 na kujikusanyia
pointi 73, wakishinda 23, sare tano na kufungwa nne.

Katika michuano ya kimataifa iliyopita, Yanga ilishindwa
kufanya vizuri na hata michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika tofauti na watani
wao wa jadi Simba waliofika hadi hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sababu kubwa zilizoibeba Simba msimu huu ni kikosi
chao kusheheni wachezaji wenye kiwango cha juu na uzoefu kama Meddie Kagere,
Erasto Nyoni, Clatous Chama na wengineo.

Share.

About Author

Leave A Reply