Saturday, August 17

Hammer Q: Sijatusua, bado naudai muziki

0


NA JEREMIA ERNEST

ZIPO nyingi ila ‘Pembe la Ng’ombe’ akiwa na Bendi ya
Dar Modern Taarab, ndiyo ngoma iliyothibitisha kuwa si tu Bongo Fleva, hata muziki
huo wa mwambao anauweza.

Huyo si mwingine, ni Hussein Mohamed ‘Hammer Q’,
ambaye alitamba zaidi katika miaka ya 2000, akitumia ngoma ya ‘Lady’
kujitambulisha Bongo Fleva.

Kipindi hicho jamaa alikuwa chini ya lebo ya Simoti
Vibe ambayo kwa sasa mashabiki wa burudani nchini wanaifahamu kama Nyumba ya
Vipaji (House of Talent – THT).

Akimbia shule kisa muziki

Msanii huyo ni mzaliwa wa Nungwi, Zanzibar, akipata elimu
yake ya msingi katika Shule ya Gububu. Baadaye, alijiunga kidato cha kwanza
hadi cha tatu katika Shule ya Sekondari Tumekuja.

“Niligundua kipaji changu cha kuimba nikiwa sekondari.
Wakati huo nilikuwa nasoma huku nafanya kazi ya kunyoa watu nywele. Hivyo, saluni
ilikuwa sehemu kubwa ya kufanyia mazoezi.

Anasema baadaye aliamua kuacha shule na kuhamia Dar
es Salaam kutafuta njia za kutoka katika muziki. “Nilikaa takribani miaka
miwili bila ya mafanikio, ndipo niliposikia kuna mashindano ya ‘Zanzibar Talent
Show’ ambayo yalikuwa yanaratibiwa na marehemu Ruge Mutahaba,” anasema.

Ruge amkutanisha na Lady Jaydee

“Nilipofika, nilikuta kambi imeshaanza siku
mbili zilizopita, hivyo aliyekuwa anasimamia aliniambia sitaweza kupata nafasi
ya kushindana.

“Nikaomba nipande jukwaani tu kuburudisha. Baada ya
kushuka jukwaani, marehemu Ruge aliniita na kuniambia alikuja Zanzibar kwa
ajili yangu kwa kuwa alisikia taarifa zangu kutoka kwa mwanzilishi wa Chuchu
Sound, Yusuf Chuchu.

“Kwa mara ya kwanza marehemu Ruge alinipatia Sh laki
moja kwa ajili ya nauli na kuniambia kesho yake niende Dar es Salaam nitamkuta
katika Jengo la Kitega Uchumi,” anasema Hammer Q.

Akiwa chini ya lebo ya Simoti Vibe ya Ruge, ndipo
alipoanza kufanya kazi na Ray C, Lady Jeydee, Man Dojo na wengine.

“Ngoma yangu ya kwanza ilikuwa ‘Jamila’ lakini
haikutamba sana ila niliifanyia shoo wakati msanii Sean Paul alipokuja kwa mara
ya kwanza nchini,” anasema na kuongeza:

“… Baada ya hapo, nilishauriwa na marehemu Ruge niimbe
taarabu kutokana na mvuto wa sauti yangu. Ndipo nikaimba ‘Pembe la Ng’ombe’
ambayo ilitamba sana.”

Hata hivyo, baada ya Simot Vibe kubadilishwa jina na
kuwa THT, aliletwa mwalimu raia wa Zaire, Mangu Stino, ambaye hata hivyo
waliishia kugombana, hivyo Hammer Q ‘kusepa’ zake.

Afunguka kilichoivunja ndoa yake

Ukimuuliza Hammer Q juu ya changamoto alizokumbana
nazo katika muziki, atakutajia ndoa yake ya mwaka 2013 na mwanamuziki mwenzake
wa Taarab, Salha, ambapo walibahatika kupata mtoto wa kiume.

“Mke wangu ilikuwa tukigombana kidogo anakwenda kwa
waandishi wa habari na kuanza kunianika kwenye redio na magazeti kwa sababu ya
umaarufu wangu. Hivyo nikaona niachane naye tu,” anasema.

Asema anaudai muziki

Akizungumzia kupotea kwake kwenye muziki, anasema
muziki umebadilika tofauti na enzi alizokuwa akitamba. Pia, alikatishwa tamaa
na baadhi ya vyombo vya habari kwa kutocheza ngoma zake kwa sababu wanazozijua
wenyewe.

“Nafanya zaidi muziki wa bendi, naimba katika hoteli
mbalimbali za kitalii,” anasema Hammer Q na kuongeza kuwa pia amekuwa akitupia
kazi zake katika mtandao wa Youtube.

Juu ya faida aliyopata kutokana na muziki, anasema
hakuna alichoambulia, hivyo hadi sasa anaudai muziki, akiamini ipo siku
utamlipa kwa kuwa ni kazi anayoitegemea kuendesha maisha yake.

Aliiambia safu hii kwa sasa anaishi Kimara, Dar es Salaam,
ambapo mbali ya kuimba pia ni prodyuza katika studio yake iliyoko huko.

Anaongeza kuwa ana ngoma nyingi nzuri lakini hawezi
kuzitoa kwa sababu hana mtu wa kumsimamia. “Muziki unahitaji mtu wa
kukusimamia, si tu kifedha, bali awe na njia mbadala nyingi. Siwezi kutoa
nyimbo zangu zikapotelea njiani,” anasema Hammer Q, akisisitiza kuwa anahitaji mtu
wa aina hiyo.

Share.

About Author

Leave A Reply