Wednesday, August 21

CHUKI TU ;Hata hawa waliwahi kugombana kama ilivyokuwa kwa Zidane, Bale

0


MADRID, Hispania

UGOMVI au kugombana kati ya kocha na mchezaji wake
ni jambo la kawaida katika soka, kama ilivyo hivi sasa macho ya kila mmoja
yameelekezwa ndani ya kikosi cha Real Madrid.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane na winga wake,
Gareth Bale, hawako kwenye maelewano kama zamani baada ya kocha huyo raia wa
Ufaransa kusema kuwa mchezaji huyo hana hadhi ya kucheza ndani ya kikosi chake
hata ingetokea akapewa nafasi ya kufanya mabadiliko ya wachezaji wanne
asingempa nafasi mchezaji huyo.

Naye Bale hakukaa kimya baada ya kocha wake kuongea
hivyo, kwani alisema kuwa ndani ya Real Madrid ana mkataba wa miaka mitatu
ambao una thamani ya pauni milioni 17, hata asipocheza ataenda kucheza gofu tu.

Juzi Real Madrid walikumbana na kichapo cha mabao
2-0 kutoka kwa Real Betis huku Bale akiishia kuangalia mchezo huo kama mchezaji
wa akiba tu.

Makala haya yanakuletea makocha ambao
waliwahi kugombana na wachezaji wao kama ilivyokuwa kwa Zidane na Bale ndani ya
kikosi cha Real Madrid.

Alan
Shearer v Joey Barton

Hawa ni wachezaji wenye historia
kubwa ndani ya kikosi cha Newcastle United, Alan Shearer, mkongwe wa kikosi
hicho alipokuwa kocha alikumbana na kiungo mtata, Joe Barton wa timu hiyo.

Ilikuwa dhidi ya Liverpool katika
Uwanja wa St. James Park, Shearer alimpa nafasi Barton ambaye hakuonyesha
kiwango kizuri kwenye mechi hiyo, wawili hao waliingia katika mzozo wa
kutupiana maneno baada ya mchezo huo.

Barton aliishia kusema: “Shearer ni
kocha wa ovyo kuwahi kutokea ambaye hajui mbinu.”

Kiungo huyo aliadhibiwa na timu yake
kwa kukatwa mshahara wa mwezi mmoja huku akifungiwa kucheza michezo mitano.

Trevor Francis v Alex Kolinko

Kipa wa Crystal Palace, Alex Kolinko ambaye
alikumbana na ngumi kali ya pua kutoka kwa kocha wake, Trevor Francis, baada ya
kucheka wakati timu yake imefungwa bao la mapema zaidi dhidi ya Bradford City
mwaka 2002.

Kipa huyo aliyekuwa benchi alisema kuwa
hakucheka sababu ya timu yake kufungwa, hata hivyo, ilizua mzozo mkubwa kati
yake na kocha ambaye hakupewa adhabu yoyote na klabu wala Shirikisho la Soka
England, FA.

Mick McCarthy v Roy Keane

Roy Keane anafahamika kwa utata wake,
hii ilitokea katika kikosi cha timu ya taifa ya Ireland wakati kinajiandaa na
fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002.

Keane hakufurahishwa na maandalizi
ya timu yake kuelekea kwenye fainali hizo kubwa duniani, alisema: “Kila mmoja
anaona uwanja wa mazoezi na jinsi mambo yanavyokwenda.”

Hiyo ilipelekea mchezaji huyo wa
zamani wa Manchester United kuingia kwenye ugomvi mzito na kocha wake, Mick
McCarthy, huku nchi nzima kupitia magazeti na vyombo vya habari vingine
vikizungumzia malumbano hayo.

Brian
Laws v Ivano Bonetti

Ivano Bonetti, alikuwa mchezaji
kipenzi kwa mashabiki wa kikosi cha Grimsby Town pia hata kwa kocha wake, Brian
Laws ambaye alimhusudu sana nyota wake.

Lakini Laws alimshushia zigo la
lawama Bonetti baada ya kukumbana na kichapo kutoka kwa Luton Town kwa
kumwambia mchezaji huyo hakujituma zaidi uwanjani.

Hiyo ilipelekea wawili hao kuingia
kwenye mgogoro mzito kiasi cha kukunjana mashati kwenye vyumba vya kubadilishia
nguo, unajua nini kilifuata? Basi Bonetti hakucheza tena pia aliuzwa mwisho wa
msimu kwenda Tranmere Rovers.

Brian
Clough v Nigel Jemson

Ni ngumu kwa kocha ambaye anapendwa
na wachezaji wake, lakini ilitokea wakati mkufunzi huyo, Brian Clough,
alipomtolea maneno ya kukera mchezaji wake, Nigel Jemson, aliyekuwa akicheza
katika kikosi cha akiba baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kwa majeraha.

Baada ya mapumziko, Clough alimwambia
mchezaji huyo asimame katika chumba cha kubadilishia nguo na kumuuliza kama
aliwahi kupigwa ngumi ya tumbo.

Jemson alijibu kuwa hakuwahi, basi
Clough alimpiga mchezaji huyo na ugomvi mkubwa kutokea kabla ya wachezaji
wengine kuamua na kuwatenganisha, ndio ulikuwa mwisho wa maelewano kati ya
wawili hao.

Share.

About Author

Leave A Reply