Monday, August 26

Bosi wa Samatta aipa Yanga vifaa

0


NA
HUSSEIN OMAR

YANGA
wamepata bonge la zali baada ya kuletewa vifaa na Meneja wa Mtanzania
anayetamba Ulaya akiitumikia klabu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta.

Meneja
huyo ni Jamal Kisongo na kwamba tayari wachezaji wameanza mazoezi jana tayari
kuona kama wanaweza kumshawishi Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, kuelekea usajili
wa msimu ujao.

Wachezaji
hao wanatoka nchi za ukanda wa Afrika Magharibi unaosifika kuwa ni nyota
wapambanaji wenye kiu ya kucheza soka la kulipwa Ulaya.

Kati
yao, wawili wanatoka nchini Nigeria, ambao ni Victor Akpan na Shehu Magaji, Alex
Komenan na Mohamed Camara, wakiwa ni raia wa Ivory Coast, ambao jana walianza
majaribio na timu hiyo katika mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha
Polisi, Kurasini, Dar es Salaam.

BINGWA
ambalo jana lilikuwapo mazoezini hapo, lilishuhudia nyota hao, watatu viungo na
mmoja mshambuliaji, wakipiga tizi la kufa mtu pamoja na vijana wa Zahera wanaojiandaa
na mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam, utakaochezwa Jumanne
ya wiki ijayo kwenye Uwanja wa Taifa.

Akizungumza
na BINGWA jana, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema wachezaji hao wapo
katika majaribio katika kipindi hiki ambacho klabu za Ligi Kuu Bara na zile za
Daraja la Kwanza zikisubiri kufunguliwa dirisha la usajili.

“Wachezaji
hawa wamekuja kufanya majaribio na kama ulivyowaona leo (jana), wameanza
mazoezi na wameletwa na Jamal Kisongo, kama wakimridhisha kocha watasajiliwa,’’
alisema Hafidh.

Kwa
upande wake, Zahera alikiri: “Hawa wachezaji wapo hapa kwa ajili ya kufanya
majaribio, watatu wanacheza nafasi ya kiungo na mwingine ni mshambuliaji… sio
hawa tu, kuna wengine wengi utawaona, subiri kuanzia kesho.”

Alisema
amekuwa akipokea simu kila kukicha kutoka kwa wachezaji wa mataifa mbalimbali
kuomba kufanya majaribio Yanga na kwamba amefungua milango kwa mchezaji yeyote
anayejiamini kuwa na uwezo wa kupata namba katika kikosi chake cha msimu ujao
kufika mazoezini aweze kumpima.

Yanga
itavaana na Azam Mei 28, mwaka huu, katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara,
utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kuelekea
katika mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amepania vilivyo kuweka
heshima kwa kushinda na kumaliza ligi kwa kishindo cha aina yake.

Katika
mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Aprili 28, mwaka huu, Wanajangwani hao
waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es
Salaam.

Bao
pekee la Yanga katika mchezo lilifungwa na Mrisho Ngassa dakika ya 13, baada ya
kumalizia pasi ya Ibrahim Ajib.

Katika
msimamo wa ligi hiyo, Yanga ipo nafasi ya pili kutokana na alama 86 walizovuna
ndani ya mechi 37, huku Azam FC yenye idadi kama hiyo ya michezo, ikishika ya
tatu kwa kukusanya pointi 72.

Share.

About Author

Leave A Reply