Tuesday, August 20

Beki Yanga awatangazia vita Msimbazi

0


WINFRIDA MTOI

BEKI wa timu ya Yanga, Andrew Vicent ‘Dante’,
ametangaza vita kwa mahasimu wao Simba akisema watakula nao sahani moja katika
kupigania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Baada ya Yanga kupoteza mechi dhidi ya Mtibwa Sugar wakifungwa
bao 1-0, Simba wapinzani wao wakubwa katika mbio za ubingwa nao walipunguzwa
kasi na Kagera Sugar.

Akizungumza na BINGWA, Dante alisema wanafahamu
wapinzani wao wana hasira ya kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kitendo ambacho
kinawafanya waelekeze nguvu zote Ligi Kuu.

Alisema Yanga inazungumziwa kwamba haipo kwenye ubora
kutokana na kutofanya vizuri katika baadhi ya michezo, lakini ukweli uliopo hawajakata
tamaa ya ubingwa hivyo watapambana hadi dakika ya mwisho.

“Simba wameondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika
na hasira zote wamehamishia Ligi Kuu wakilenga zaidi kutetea ubingwa wao, hivyo
lazima watacheza mechi zao kwa kasi,” alisema Dante.

Dante aliongeza kuwa wakati Simba wanapambana wakumbuke
kuwa Yanga pia wapo katika mapambano, hivyo kila mmoja atahesabu alichokivuna mwishoni
mwa ligi.

“Sisi tumecheza mechi nyingi kuliko wao ila najua kuna
sehemu tutawakamata, Simba hawawezi kushinda michezo yote ya viporo kwa sababu
kipindi hiki mechi zote ni ngumu maana kila timu inahitaji matokeo ya ushindi,”
alisema Dante.

Hata hivyo, beki huyo alikiri kwamba wanatambua wanakabiliwa
na mechi ngumu na kila mmoja anakiangalia kikosi chao kwa jicho la tofauti, lakini
amewataka wafahamu bado wapo katika mbio za ubingwa wakichuana na Wekundu wa
Msimbazi.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Yanga inashika usukani ikiwa
imevuna pointi 74 baada ya kucheza mechi 32 ambapo wameshinda 23, sare tano na
kufungwa nne.

Kwa upande wa Simba wao wanashika nafasi ya tatu baada
ya kujikusanyia pointi 60, wakiwa wameshuka dimbani mara 24 na kushinda 19,
sare tatu na kufungwa mbili.

Share.

About Author

Leave A Reply