Friday, July 19

Mo Dewji aongoza kikao cha kwanza Bodi ya Wakurugenzi Simba

0
Mwekezaji mtarajiwa wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ leo amefanya kikao cha kwanza cha Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo.

MO Dewji amekutana na viongozi hao ikiwa ni wiki moja baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa klabu hiyo jijini Dar es Salaam.

Mo Dewji aliongoza kikao hicho kilichohudhuria na  Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, Mwenyekiti Swedi Mkwabi na wajumbe, Dk Zawadi Kadunda, Seleman Haroub, Hussein Kitta, Asha Baraka na Mwina Kaduguda waliochaguliwa wiki iliyopita.

Wengine ni kaimu Rais wa zamani wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, wajumbe Said Tulliy, Musley Al- Ruwey na Mlamu Nghambi.

Hata hivyo uongozi wa Simba ulitoa picha za wajumbe na Mo kukutana katika mitandao yake ya jamii  bila ya kutoa taarifa yoyote juu ya mkutano huo wa leo.

Viongozi hao wamekutana ikiwa ni siku moja baada ya Shirikisho la Soka Africa (CAF), kutangaza ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba kupangwa dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland.

Katika ratiba hiyo, wawakilishi hao wa Tanzania wataanza kwa kukipiga na Mbabane Swallows ya Swaziland katika mchezo wa kwanza ambao Simba itaanzia nyumbani.

Mbabane inakumbukwa baada ya kuitupa nje Azam FC katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika katika raundi ya kwanza mapema mwaka 2017.

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa mchezo michezo ya kwanza itachezwa kati ya Novemba 27 na 28 na baada ya hapo itacheza mchezo wa marudiano ugenini kati ya Desemba 4 na 5 mwaka huu.

Mshindi wa jumla wa mechi hiyo atakutana na mshindi wa mchezo baina ya Nkana Red Devils ya Zambia na UD Do Songo ya Msumbiji ili kusaka timu itakayofuzu hatua ya makundi.

Katika mashindano hayo pia JKU ya Zanzibar itaanzia nyumbani itakapoivaa Al Hilal ya Sudan na mshindi wa jumla wa mechi hiyo atakutana na mshindi wa mechi baina ya APR ya Rwanda na Club Africain ya Tunisia.

Kwenye Kombe la Shirikisho, Mtibwa Sugar imepangwa kukutana na Northern Dynamo ya Shelisheli na mshindi wa mechi hiyo atacheza na KCCA ya Uganda wakati Zimamoto ya Zanzibar itaanza na Kaizer Chief ya Afrika Kusini na ikishinda mchezo huo itakutana na mshindi wa mechi kati ya El Geco ya Madagascar na Deportivo Unidado ya Guinea ya Ikweta.

Advertisement

tang

==

Advertisement

Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==

….

===

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )

Share.

About Author

Leave A Reply