Friday, August 23

WAZIRI MKUU WA MALI PAMOJA NA BARAZA LAKE WAJIUZULU

0


Bamako, MALI.

Kutoka nchini Mali Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Soumeylou Boubeye Maiga pamoja na baraza lake la mawaziri wamewasilisha barua ya kujiuzulu kufuatia kura ya kutokuwa na imani nao iliyopigwa mapema leo Ijumaa baada ya kutokea mauaji kwenye kijiji kimoja katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Hatua ya serikali hiyo ya Mali kujiuzulu inafuatia baada ya wafugaji wapatao 160 wa jamii ya Fulani kuuawa na kundi la wanamgambo walio msituni mwezi uliopita.

Taarifa iliyotolewa muda mfupi uliopita na ikulu ya nchi hiyo imesema, Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita, amepokea barua hiyo ya kujiuzulu kwa Maiga na mawaziri wake na kusema kuwa waziri mkuu mpya atatangazwa hivi karibuni na serikali mpya kuundwa baada ya mashauriano na wanasiasa wa chama tawala na upinzani.

Serikali ya Mali imelaumiwa kwa kushindwa kukabiliana na wanamgambo waliotekeleza mauaji hayo. Mauaji ya wafugaji hao wa jamii ya Fulani yaliyotokea mnamo Machi 23 yameelezwa kuwa mabaya zaidi katika historia ya hivi karibuni ya nchi hiyo.

Kufuatia kuongezeka kwa vitendo hivyo vya kikatili nchini Mali pamoja na kuuawa wafugaji wa jamii ya Fulani na waasi, Rais Keïta alitangaza kumfuta kazi mkuu wa majeshi na kamanda wa kikosi cha ardhini katika nchi hiyo.

Mauaji hayo ya wafugaji wa jamii ya Fulani yalitokea baada ya wiki moja kutokea shambulizi la kigaidi dhidi ya kambi moja ya kijeshi lililosababisha jumla ya askari 23 kuuawa.

Kundi moja la kigaidi na ukufurishaji lenye mahusiano na genge la al-Qaidah lilitangaza kuhusika na shambulizi hilo, ambapo raia wa Mali wamekuwa wakilalamikia udhaifu wa jeshi la nchi hiyo na wamelitaka lidhibiti vitendo vya jinai na mauaji pamoja na kuwalinda.

Licha ya wanajeshi 4500 wa Kifaransa kuwepo katika eneo la Sahel mwa Afrika, lakini mashambulizi ya kigaidi yameshika kasi katika eneo hilo. Walinda amani hao walifika eneo hilo mwaka 2013 kwa ajili ya kupambana na ugaidi.


Share.

About Author

Leave A Reply