Sunday, August 25

UPINZANI ALGERIA WASUSIA MAZUNGUMZO NA KIONGOZI WA MUDA WA NCHI HIYO BENSALAH

0


Algers, ALGERIA.

Vyama vya upinzani nchini Algeria hapo jana vilisusia mazungumzo yaliyoandaliwa na kiongozi wa muda nchini Algeria Abdelkader Bensalah, ili kujadili juu ya uwezekano wa kuahirisha uchaguzi mkuu uliopangwa Julai 4 mwaka huu.

Vyama hivyo vya kisiasa nchini humo viliamua kususia mkutano huo, kufuatia kile vilisema ni mkutano ambao unaenda kinyume na matakwa ya Wananchi.

“Wananchi wa Algeria wanataka mabadiliko halisi. Hawakubaliana kwamba utawala uendelee kuongozwa na watu waliokuwa chini ya uongozi wa utawala wa rais Abdelaziz Bouteflika,

“Sote tunaomba Bensalah kuondolewa kwenye nafasi hiyo, anapaswa kuondoka. Ni vizuri kusikia wito wa wananchi wa Algeria na kisha tutaketi kwenye meza ya mazungumzo.” amesema Abderrazak Makri kiongozi wa chama cha MSP.

Kiongozi wa muda nchini Algeria Abdelkader Bensalah, ambaye aliteuliwa hivi karibuni kumrithi rais Abdelaziz Bouteflika, hivi karibuni aliunda kamati maalum ambayo kwa mara ya kwanza hapo jana Jumatatu iliitisha kikao kujadili juu ya uwezekano wa kuahirisha uchaguzi mkuu uliopangwa Julai 4 mwaka huu.

Maandamano yameendelea kushuhudiwa nchini Algeria ambapo wananchi wameomba kuondolewa kwa mfumo wote wa utawala uliokuwa chini ya rais aliyelazimishwa kujiuzulu, Abdelaziz Bouteflika.


Share.

About Author

Leave A Reply