Sunday, August 25

RIEK MACHAR AMGEUKA RAIS SALVA KIIR WA SUDAN KUSINI, AKATAA KUREJEA NCHINI

0


Juba, SUDAN KUSINI.

Kiongozi wa upinzani nchini Sudan Kusini, Riek Machar, amesema hayuko tayari kurejea nchini mwake kwa sasa, huku akitoa mwito wa kuahirishwa mchakato wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Msemaji wa chama cha SPLM-IO, Puot Kang Chol, chama chake Machar amesema kiongozi huyo wa upinzani hayuko tayari kurejea nchini humo kwa sasa na mpango wake wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa umeahirishwa kwa muda wa miezi sita zaidi.

Bw Kang Chol amebainisha kuwa, Machar hawezi kurejea Juba bila kudhaminiwa usalama wake, huku akikanusha madai kuwa wanajeshi wapatao 3,000 wa serikali na upinzani wanafanya mazoezi ya pamoja, ikiwa ni sehemu ya mkakati huo wa kuunda serikali jumuishi.

Machar alitazamiwa kurejea nchini Sudan Kusini mwezi ujao wa Mei, chini ya makubaliano ya amani yaliyosainiwa baina yake na Rais Salvaa Kiir mwezi Septemba mwaka jana huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, makubaliano ya kwenda kuchukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hiyo.

Alhamisi ya wiki iliyopita, mahasimu hao wawili wa kisiasa wa Sudan Kusini walikutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu mwezi Septemba mwaka jana, katika mkutano wa Vatican, Makao Makuu ya Kanisa Katoliki mjini Rome, Italia.

Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis, ambaye alikuwa mwenyeji wa Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir pamoja na hasimu wake Riek Machar aliwaasa viongozi hao kuendeleza mazungumzo ya amani licha ya ugumu wake.

Nchi ya Sudan Kusini iliyojitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani, mnamo Desemba mwaka 2013 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi.

Share.

About Author

Leave A Reply