Saturday, August 17

KATIBA YA MISRI YABADILISHWA KWA KURA, SASA RAIS KUTAWALA MPAKA 2030

0


Cairo, MISRI.

Kura ya maoni ambayo imekuwa ikifanyika nchini Misri tokea tarehe 20 Aprili ilikamilika Jumatatu usiku ambapo Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo imetangaza kwamba ushiriki wa wananchi ulikuwa wa asilimia 44.33 na mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo yamepitishwa kwa asilimia 88.

Baada ya kufanyiwa marekebisho baadhi ya vipengee vya katiba ya Misri, sasa Rais Abdulfattah as-Sisi wa nchi hiyo anaweza kuendelea kutawala hadi mwaka 2030.

Hivi karibuni bunge la Misri lilirekebisha kipengee cha 140 cha katiba hiyo, ambapo kipindi cha urais wa nchi hiyo kimerefushwa kutoka miaka 4 hadi 6. Kwa mujibu wa marekebisho hayo sasa Rais wa Misri atakuwa na fursa ya kuongoza vipindi viwili vya miaka 6 kila kimoja.

Mbali na kurefushwa kipindi cha urais, Seneti ya nchi hiyo iliyofutwa mwaka 2011 kufuatia malalamiko ya wananchi dhidi ya dikteta Husni Mubarak imerudishwa tena, rais kupewa mamlaka makubwa ya kuwateua majaji na wanawake kupewa asilimia 25 ya viti vya bunge.

Awali wapinzani wa serikali walipinga vikali kufanyiwa marekebisho katiba hiyo wakisema kuwa lengo la serikali lilikuwa ni kuendelea kumbakisha as-Sisi madarakani.

Rais Sisi aliingia madarakani baada ya kumpindua kijeshi Rais Muhammad Mursi mwaka 2013. Katika kipindi hicho as-Sisi alikuwa Waziri wa Ulinzi. Alihodhi madaraka ya nchi hiyo baada ya kuandaa uchaguzi wa kimaonyesho mwaka uliofuata wa 2014.

Tokea wakati huo hadi sasa as-Sisi amekuwa akitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa kuwakandamiza wapinzani wa serikali kutokana na uungaji mkono mkubwa anaopata kutoka kwa nchi za Magharibi na hasa Marekani.


Share.

About Author

Leave A Reply