Sunday, August 18

BOBI WINE AFUNGULIWA MASHTAKA YA KUFANYA MAANDAMANO BILA KIBALI

0


Kampala, UGANDA.

Jeshi la Polisi nchini Uganda linamshikilia tangu jana Jumatatu Mbunge machachari wa upinzani Robert Kagyulanyi maarufu kama Bobi Wine na tayari limemfunguliwa mashtaka.

Mmoja wa wanasheria wa Mbunge huyo amewaambia waandishi wa habari mjini Kampala kwamba, mteja wake amekamatwa kwa sababu za kisiasa.

Hata hivyo serikali ya Uganda kupitia kwa mmoja wa wasemaji wake imeeleza kwamba, Mbunge Bobi Wine pamoja na watu wengine wanaopenda kuandamana bila kufuata sheria hawataachwa na mkono wa sheria.

Taarifa ya serikali ya Uganda imeeleza kwamba, Mbunge huyo na wapinzani wengine wanashikiliwa baada ya kufanya maandamano kinyume cha sheria.

Bobi Wine ambaye amejizolea umashuhuri katika miezi ya hivi karibuni, alipandishwa kizimbani katika mahakama moja jijini Kampala na kusomewa mashtaka ya kuandaa mkutano na kufanya maandamano kinyume cha sheria mwaka 2018 na baadaye kuzuiwa katika Gereza la Luzira kabla ya kuachiliwa huru baadaye.

Hivi karibuni polisi ya Uganda ilipiga marufuku tamasha lolote la muziki la Mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki hatua ambayo inatajwa na wapinzani nchini humo kwamba, inalenga kukwamisha harakati za Mbunge huyo.

Aidha, imeelezwa kuwa, wakati mataifa kadhaa ya ukanda wa Afrika Mashariki yakijiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu, wadadisi wa mambo wanaona kuwa, huenda katika chaguzi zijazo vyama vya upinzani vikakosa ushawishi na nguvu na hata baadhi yao kufa hasa kutokana na ukandamizaji dhidi ya wapinzani hususan katika nchi za Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.


Share.

About Author

Leave A Reply