Friday, April 19

JAJI NSEKELA AWATAKA VIONGOZI KUWA MAKINI NA TAARIFA WANAZOJAZA KATIKA MATAMKO YAO

0


index

Kamishna wa Maadili Jaji (Mst) Harold Reginald Nsekela akiongea na viongozi wa umma kuhusu umakini wakati wa ujazaji iwa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa hivi karibuni

……………………….

Viongozi wa umma wametakiwa kuwa makini na taarifa zao wanazojaza katika Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa sababu taarifa zao ni nyeti na ujazaji wake ni jambo la Kikatiba.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Kamishna wa Maadili Jaji (Mst.) Harold Nsekela kwa nyakati tofauti hivi karibuni alipokutana na viongozi wa mikoa ya Mtwara na Iringa.

Alisema, taarifa za Tamko ni zako binafsi nani nyeti, ukimpa mtu asiyehusika kuniletea tamko taarifa zako zikivuja utanilalamikia mimi?”

“Leteni Matamko yenu nyinyi wenyewe msihatarishe siri zenu. Nyinyi ni watu wakubwa katika nchi hii, siri zenu zikivuja mtahatarisha heshima ya taifa letu kwasababu mmepewa dhamana kubwa ya kuwaongoza wananchi,” alisema. Mhe. Nsekela

Baadhi ya viongozi wa umma wamekuwa na tabia ya kuwatuma watu wasiohusika kuleta matamko yao katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili kila ifikapo Desemba 31 ya kila mwaka.

“Kujaza fomu ni jambo la Kikatiba na lazima lipewe uzito unaostahili. Kwa hiyo mnapojaza Fomu za Tamko la Raslimali na Madeni kuweni makini na taarifa mnazojaza, semeni ukweli katika Matamko yenu kwasababu baadhi yenu mnakuja kujazia fomu zenu ofisini kwangu, hivyo siamini kiongozi wa namna hii kama ana maadili,” alisema Mhe. Nsekela.

Kwa mujibu wa Kamishna Nsekela, kujazia Fomu za Tamko la Raslimali na Madeni katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kitendo cha kuidharau Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ofisi husika kwa ujumla.

“Siamini kiongozi wa namna hii kama ni mtu makini na mwenye maadili kwa sababu katika fomu hizi kuna nafasi ya mwenza wake na watoto wenye umri chini ya miaka 18. Ukijazia tamko lako ofisini kwangu taarifa za mwenza wako utazijaza saa ngapi wakati hukuambatana naye?”alihoji Mhe. Nsekela.

Kamishna Mhe. Nsekela ameagiza Wakuu wa Kanda wanaosimamia Ofisi za Sekretarieti ya Maadili kuwaita viongozi wote waliojazia matamko yao katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili kuja kwa gharama zao na kuwahoji kuhusu mali zao walizojaza katika matamko yao kwa kulinganisha tamko la mwaka 2018 na matamko ya miaka ya nyuma.

Ibara ya 132 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  inaeleza kuwa, Kutakuwepo na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo itakuwa na mamlaka ya kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya sheria ya Maadibli ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo.

Ibara ya 132 (5) (b) inaeleza kuwa, itawataka watu wanaoshika nafasi fulani za madaraka kutoa mara kwa mara maelezo rasmi kuhusu mapato, rasilimali na madeni yao.

Kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 kifungu cha 9 (1) (a) na (b) kila kiongozi wa Umma anatakiwa kuwasilisha Tamko lake la Rasilimali na Madeni siku 30 baada ya kuteuliwa na kila ifikapo tarehe 31 Desemba ya kila mwaka.

Share.

About Author

Leave A Reply