Wednesday, December 12

WAZIRI UMMY ATOA ONYO KWA WAUGUZI WANAOVUNJA MAADILI YA KAZI

0Na WAMJW – Nanyumbu, Mtwara

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu ametoa onyo Kali kwa Wauguzi wote kwenye vituo vya  kutolea huduma za afya nchini wanaovunja maadili na miiko ya kazi za uuguzi ikiwemo matumizi ya lugha chafu kwa wagonjwa na wanaowapiga akina mama wajawazito wakati wakijifungua.

Ameyasema hayo  wakati alipotembelea Hospitali ya Wilaya Nanyumbu, akiwa katika ziara yake Mkoani Mtwara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya na uhamasishaji kwa wananchi juu ya umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya hasa katika msimu huu wa Biashara ya Korosho.

Waziri Ummy alisema kuwa Serikali kupitia Baraza la Uuguzi litawafutia usajili Muuguzi yeyote atakayegundulika ametenda kosa la kumpiga mama mjamzito au kumtolea lugha chafu wakati wa kujifungua.

“Tunataka kumjua huyo, ambae ni hodari sana wakupiga wanawake wajawazito, makofi wakati wakujifungua, kwa kweli huyo ni wa kumfukuza kazi, Mimi mkiniletea namfutia Leseni yake kabisa, hafanyi kazi Serikalini, hafanyi kazi Sekta Binafsi” alisema Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy alitoa Maagizo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe.Hamis Dambaya kuhakikisha  Wauguzi na Watumishi wote wanavaa vitambulisho vya kazi wakati wote wakiwa eneo la kazi ili wananchi wanaokwenda kupata huduma za Afya waweze kuwatambua majina yao.

“Tumewaambia wavae vitambulisho, ili mtusaidie kutaja jina la Wauguzi wanaovunja maadili ya kazi zao, hapa naomba nisiwahukumu wote, Mganga Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi mpo hapa, nikirudi tena nisisikie kuna Muuguzi anapiga makofi wajawazito wanaokuja kujifungua” alisema Waziri Ummy.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya italeta mashine mpya ya kisasa ya digitali ya X-Ray ndani ya miezi mitatu itayosaidia wananchi wa Nanyumbu hasa kutokana na Wilaya hiyo kuwa katika Bara bara kuu ya kutoka Masasi hadi Songea.

Aidha, Waziri Ummy ametoa Rai kwa wananchi wa Nanyumbu kuhakikisha kabla ya kufika Disemba 31 mwaka huu, kaya zote katika eneo hilo lazima liwe limejenga na kutumia choo bora ili kupunguza magonjwa ya Bakteria yanayoigharimu Serikali pesa nyingi katika matibabu na Dawa.

“Ndugu zangu nendeni pale Hospitali, katika kila Wagonjwa 100, Wagonjwa 60 wana magonjwa ya kuhara,magonjwa ya tumbo, magonjwa yanayohusiana na kiwango duni cha usafi, nimekuwa nikiimba wimbo huu tangu nikiwa Waziri wa Afya, na hapa tulipofikia ni agizo la Waziri Mkuu pindi alipokutana na maafisa Afya wa Halmashauri na Mkoa jijini Dodoma” alisema Waziri Ummy

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa akiwa kama Waziri wa Afya kazi kubwa aliyonayo ni kuhakikisha anawakinga watu wasiumwe na pale wanapoumwa waweze kupata Huduma Bora za Afya, lazima niwe mkali kwenye kinga, mimi ni Waziri wa Afya sio Waziri wa Wagonjwa” alisema Waziri Ummy.

Share.

About Author

Leave A Reply