Monday, March 18

WANANCHI WA KIJIJI CHA NDUNYUNGU WILAYANI LIWALE WASIMAMISHA MSAFARA WA AWESO; WATAKA MRADI UKAMILIKE HARAKA

0


Wananchi wa kijiji cha Ndunyungu kilichopo Wilayani Liwale Mkoani Lindi wamelazimika kusimamisha msafara wa Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso alipokuwa njiani kwenda kukagua mradi wa maji wa Barikiwa Wilayani humo.

Wakiwa na mabango yaliyobeba ujumbe wa kumtaka Nambu Waziri awasaidie kupata maji, pia walieleza adha inayowakumba ya kusubiria maji kwa muda mrefu katika eneo wanalochetea maji jambo ambalo linawasababishia kuchelewa kufanya shughuli za kimaendeleo.

Baada ya kuwasikiliza kero zao Mheshimiwa Aweso alilazimika kwenda kuona chanzo pekee ambacho wananchi hao wanapata huduma ya maji, ambapo alijionea kisima kinachotumia pampu ya kusukuma kwa mkono na kuongea na wananchi walijitokeza kwa wingi.

Naibu Waziri Aweso alisema kuwa tayari mkandari anayejenga mradi kwa ajili ya kijiji hicho ameshalipwa pesa kiasi cha shilingi milioni mia moja na moja, hivyo hana sababu za kutokukamilisha mradi na kutokulipa vibarua waliochimba mitaro ya kufukia mabomba ya maji.

Aidha, akiwa katika kijiji cha Barikiwa swala la kutokulipwa kwa vibarua waliojenga mradi pia liliibuka jambo ambalo lilimlazimu Naibu Waziri kumsimamisha Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Liwale kujibu hoja za wananchi.

Mheshimiwa Aweso alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Liwale awasimamie wananchi hao walipwe kabla ya mwisho wa wiki ijayo. Naibu Waziri bado yupo Mkoani Lindi kwa ziara ya kikazi kwa kukagua miradi ya maji.

Naibu Waziri wa maji Juma Aweso akipampua maji katika kijiji cha Ndunyungu Liwale
Naibu Waziri wa Maji Juma Aweso akiwahutubia wananchi wa Barikiwa wilayani Liwale

Share.

About Author

Leave A Reply