Friday, April 19

WANAFUNZI WALIOONGOZA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE 2018 SIMIYU WAKIRI KAMBI ZA KITAALUMA ZIMEWASAIDIA

0


Mwanafunzi kutoka Shule ya Kata Nkololo aliyefanya vizuri kwa kupata daraja la kwanza (pointi saba) na kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne mwaka 2018 Ibrahimu Buyungumya(kushoto) na Mwanafunzi wa Kike Kwandu Maduhu kutoka Shule ya Sekondari Biashara aliyefanya vizuri kwa kupata daraja la kwanza (pointi 11) katika mtihani huo na kuongoza kimkoa (wasichana), wakionesha kadi zao za akaunti ambazo wamekabidhiwa (katika hafla maalum ya kuwapongeza iliyofanyika shule ya Sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari13, 2019 ) baada ya kufunguliwa akaunti na kuwekewa zawadi hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(katikati) akizungumza jambo na Mwanafunzi kutoka Shule ya Kata Nkololo aliyeongoza kimkoa katika mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne mwaka 2018 kwa kupata daraja la kwanza(pointi saba) ,Ibrahimu Buyungumya(kushoto) na Mwanafunzi wa Kike Kwandu Maduhu kutoka Shule ya Sekondari Biashara aliyeongoza kwa upande wa wasichana kwa kupata daraja la kwanza (pointi 11) katika mtihani huo, baada ya hafla ya kuwapongeza walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kimkoa, iliyofanyika katika shule ya sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari 13, 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(mwenye suti kulia) akishuhudia wanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Nkololo wilayani Bariadi wakifanya mazoezi kwa vitendo wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika Mtihani wa Kidato cha nne mwaka 2018 iliyofanyika kimkoa shuleni hapo, Februari 13, 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akiteta jambo na Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest Hinju, wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika Mtihani wa Kidato cha nne mwaka 2018 iliyofanyika kimkoa, katika shule ya sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari 13, 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(wa pili kushoto) akiwakabidhi zawadi ya ngao viongozi wa Halmashauri ya mji wa Bariadi ambayo iliongoza kimkoa na kushika nafasi ya tisa kati ya halmashauri zaidi ya 185 nchini katika mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne mwaka 2018, (kushoto na wa pili kushoto) ni wanafunzi walifanya vizuri Kimkoa kutoka shule za Serikali), wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani huo iliyofanyika kimkoa katika shule ya sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari 13, 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa nne kushoto mbele) katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa na Halmashauri ya Mji wa Bariadi , walimu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, wanafunzi walawili walioongoza katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2018 Kimkoa na wazazi wao, baada ya hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani huo iliyofanyika kimkoa katika shule ya sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari 13, 2019.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo akizungumza na viongozi, walimu, wazazi na wanafunzi katika hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika Mtihani wa Kidato cha nne mwaka 2018 iliyofanyika kimkoa, katika shule ya sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari 13, 2019.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Biashara Mwalimu Mathias Joseph akionesha zawadi ya shilingi 460,000/= iliyotolewa kama motisha kwa walimu wa shule hiyo waliofanikisha kutoa jumla ya alama A 23 katika Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha nne mwaka 2018, wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani huo iliyofanyika kimkoa katika shule ya sekondari Nkololo wilayani Bariadi Februari 13, 2019.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Wanafunzi wa shule za Serikali (kata) Wilayani Bariadi, Ibrahim Buyungumya kutoka Shule ya Sekondari Nkololo , aliyepata daraja la kwanza alama (points) saba na Kwandu Maduhu wa Biashara Sekondari aliyepata daraja la kwanza alama kumi na moja, wamekiri kuwa kambi za kitaaluma zimechangia kuongeza ufaulu wao katika Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2018.

Wanafunzi hao wameyasema hayo katika hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika Matokeo ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne mwaka 2018 Kimkoa na kuufanya mkoa kushika nafasi ya Tisa Kitaifa, iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Nkololo wilayani Bariadi, Februari 13, 2019.

Wanafunzi hao wamesema pamoja na kumuomba Mungu, juhudi zao binafsi za kujisomea, jitihada za walimu, malezi kutoka kwa wazazi wanakiri kambi za kitaaluma zilizofanyika mkoani Simiyu kwa madarasa yote ya mitihani ziliwasaidia kuwaandaa na mtihani huo wa Taifa, huku wakisisitiza kambi hizo ziwe endelevu na wakapendekeza kuwa kwa mwaka 2019 ziongezewe muda na zianze mapema zaidi.

“ Namshukuru Mungu kunifanikisha kupata daraja la kwanza alama saba, nawashukuru walimu wangu, wazazi wangu kwa namna walivyokuwa msaada kwangu; pia kipekee namshukuru Mkuu wetu wa Mkoa kwa kutuletea kambi, zimetusaidia sana maana tulipata nafasi ya kukutana na wanafunzi wenzetu na walimu mahiri kutoka shule mbalimbali na zilitusaidia kuelewa masomo kwa mawanda mapana zaidi” alisema Ibrahimu Buyungumya.

“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupata daraja la kwanza alama 11, nawashukuru wazazi, walimu pia nashukuru uwepo wa kambi za kitaaluma ambazo zilitusaidia sana kujiandaa vema na mtihani wetu, nashauri kambi hizi zianze mapema na muda uongezwe ili ziwasaidie wadogo zetu wafaulu vizuri zaidi yetu sisi” alisema Kwandu Maduhu.

Mkuu wa Shule ya sekondari Biashara, Mwl. Mathias Joseph ambaye shule yake ilifanya vzuri kwa kupata alama A 23 na alama B 79 amesema pamoja na kambi za kitaaluma siri nyingine ya kufanya vizuri ni jitihada zilizofanywa na walimu pamoja na usimamizi mzuri wa mikakati iliyowekwa na idara ya Elimu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi na mitihani ya mara kwa mara.

Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza walimu waliofanikisha na wanafunzi waliofanya vizuri katika Matokeo ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne mwaka 2018 katika mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewapongeza viongozi, walimu, wanafunzi, wazazi na wadau wote wa elimu mkoani humo, kwa jitihada walizofanya katika kuongeza ufaulu.

Aidha, Mtaka ameelekeza kamati zote za shule zikutane na wazazi wa wanafunzi wa madarasa ya mtihani ili wakubaliane juu ya wanafunzi hao kuanza kambi za kitaaluma na wazazi hao wachangie chakula ambacho watoto wao wangekula wakiwa majumbani kwao kitumike wakiwa kambini.

“Nilishatoa maelekezo na nayarudia; kamati za shule zikae na wazazi wakubaliane madarasa yote ya mtihani watoto waanze kambi za kitaaluma na wazazi wachangie chakula kile kile ambacho watoto wangekula wakiwa nyumbani, ili watoto wapate nafasi nzuri ya kusoma na kujiandaa na mtihani wa Taifa” alisema Mtaka.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Enock Yakobo ametoa wito kwa wazazi mkoani humo kuhimiza watoto kusoma ili waweze kufikia ndoto zao akakemea tabia ya baadhi ya wazazi kuwaachisha masomo watoto wa kike na kuwaozesha.

Jumla ya wanafunzi 7094 kati yao wavulana ni 4224 na wasichana 2875 walifanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2018 mkoani Simiyu na kuwezesha mkoa kushika nafasi ya tisa Kitaifa kati ya mikoa 31, ambapo umepanda kwa nafasi mbili ikilinganishwa na mwaka 2017 ambapo ulishika nafasi ya 11 Kitaifa.

Katika pongezi zilizotolewa kwa walimu na wanafunzi mwanafunzi wa kiume aliyeongoza Kimkoa amezawadiwa shilingi milioni Moja, mwanafunzi bora wa kike shilingi laki tano (wote wamefunguliwa akaunti) na kuahidiwa kupewa mahitaji yote muhimu watakapochaguliwa kidato cha tano, huku walimu sitini kila mwalimu akipewa shilingi elfu ishirini kwa kila alama A iliyopatikana kwenye somo lake.

Share.

About Author

Leave A Reply