Friday, April 19

MAWAZIRI WATANO WATEMBELEA MRADI WA KUFUA UMEME STIEGLER’S GORGE

0


Waziri wa Nishati, Medard Kalemani akizungumza na baadhi ya Mawaziri pamoja na Makatibu wakuu waliofanya ziara jana ya kutembelea mradi wa kufua umeme wa Mto Rufiji kwa ajili ya kukagua Miundombinu Wezeshi ikiwemo maji, barabara, umeme pamoja na nyumba za watumishi kabla ya kumkabidhi Mkandarasi huyo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bwawa la kuzalisha Umeme.

Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Mkazi, Mhe. William Lukuvi akiwa ameshika moya nguzo za umeme zilizotengenezwa kwa zege yenye urefu wa mita 17 ambazo zimewekwa katika Pori la Akiba la Selous ili wanyama kama vile tembo na twiga waziweze kuziangusha wakati Mawaziri watano walipofanya ziara katika mradi huo wa kufua umeme wa mto Rufiji mkoani Morogoro. Wengine wanaoangalia ni mawaziri na makatibu wakuu.

Mratibu wa Mradi wa Kufua Umeme wa Mto Rufiji, Mhandisi Justus Mtolela akizungumza na Mawaziri pamoja na viongozi mbalimbali walioambatana na katika Pori la Akiba la Selous kabla ya kuanza kufanya ziara ya kukagua Miundombinu Wezeshi katika mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe, Constantine Kanyasu akizungumza na Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi baada ya kukagua Nyumba za kuishi watumishi wanaokuja kufanya kazi katika mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji wakati Mawaziri hao walipofanya ziara jana Mkoani Morogoro ya kukagua Miundombinu Wezeshi kwa ajili ya Mkandarasi kuanza kazi.

Mratibu wa Mradi wa Kufua Umeme wa Mto Rufiji, Mhandisi Justus Mtolela akitoa maelezo kwa Mawaziri pamoja na viongozi mbalimbali walioambatana nao katika Pori la Akiba la Selous wakati wakiangalia daraja amabalo linatakiwa kujengwa upya kutokana na daraja hilo kuwa na uwezo mdogo wa kuhimili mzigo mizito itakayoanza kusafirishwa na Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa mto Rufiji mkoani Morogoro.

Baadhi ya Mawaziri pamoja na viongozi wengine wakikagua Nyumba za kuishi watumishi watakaokuja kufanya kazi katika mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji wakati wa ziara iliyofanyika katika Pori la Akiba la Selous mkoani Morogoro

Baadhi ya Mawaziri pamoja na viongozi wengine wakiangalia sehemu ya kujengwa Bwawa la kufua umeme katika mto Rufiji wakati Mawaziri hao walipofanya ziara jana katika Pori la Akiba la Selous Kanda ya Matambwe mkoani Morogoro

Eneo la Fuga ni sehemu ambayo mizigo itakuwa ikitelemshwa kwa njia ya reli itakayotumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi kufua umeme katika mto Rufiji katika Pori la Akiba la Selous katika Kanda ya Matambwe mkoani Morogoro.(PICHA ZOTE NA LUSUNGU HELELA)

NA.LUSUNGU HELELA-MOROGORO

Serikali imesema maandalizi ya miundombinu wezeshi kabla ya kumkabidhi Mkandarasi aliyepewa kazi katika Mradi wa kufua umeme wa Mto Rufiji tayari imekamilika kwa asilimia themanini.

Miundombinu hiyo ni pamoja na maji, umeme, barabara pamoja na nyumba za kukaa wafanyakazi.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mawaziri wa Wizara tano kutoka Nishati, Maliasili na Utalii, Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Fedha na Mipango baada ya kutembelea na kujionea miundombinu hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa imeshakamilika.

Ziara hiyo katika Pori la Akiba la Selous kanda ya Matambwe mkoani Morogoro iliongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani ikilenga kukagua hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ili kumuwezesha Mkandarasi kuanza kusafirisha mizigo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

Alisema kukamilika kwa miundombinu hiyo kutamuwezesha Mkandarasi huyo kuanza maandalizi ya awali ikiwemo kuanza kusafirisha mizigo kuileta katika maeneo ya ujenzi wa bwawa.Aliongeza kuwa kutokana na Mkataba uliopo Mkandarasi huyo ataanza kazi rasmi Juni 15 mwaka huu na ataukamilisha mradi huo ifikapo mwezi April 2022. 

Katika upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu alitoa tahadhari kwa wafanyakazi wanaokuja kufanya kazi katika mradi huo wasiende kupumzika vichakani kuna wanyama wakali kama vile Simba, Nyati pamoja na tembo.

” Wale wenye tabia ya kujipumzisha vichakani baada ya kufanya kazi chonde chonde jiepusheni na haya mazoea la sivyo mtaliwa na Simba.Aidha, Mhe.Kanyasu alitumia fursa hiyo kuiomba Wizara ya Utumishi kutoa kibali cha kuajiri Askari Wanyamapori zaidi ya 200 ambao watatoa ulinzi kwa Wafanyakazi wa mradi huo,

Ombi hilo linakuja kufuatia Askari wanyamapori 115 kutoka mapori mengine kuhamishiwa kwa muda katika Pori hilo katika kanda ya Matambwe kwa lengo la kuongeza nguvu baada ya askari 115 waliokuwepo kuonekana hawatoshi.

Hata hivyo , Mhe.Kanyasu alisema hatua za haraka zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja kutengeneza vyoo, malazi pamoja na maji kwa vile miundombinu iliyokuwepo katika Kanda hiyo ilikuwa na uwezo wa kuhudumia Askari Wanyamapori 85 tu lakini hadi hivi sasa kuna jumla ya askari 230.

Kukamilika kwa mradi huo wa kufua umeme, Bwawa hilo la Rufijin litakuwa la nne kwa ukubwa kwa Afrika na la kwanza kwa Afrika Mashariki, Duniani ni la 60 katika ya mabwawa sabini makubwa.

Share.

About Author

Leave A Reply