Saturday, August 17

JIACHIE: WAAJIRI WANAOTUHUMIWA KUTOJISAJILI MFUKO WA FIDIA KORTINI

0


Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.

WAAJIRI  wa kampuni nne tofauti wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini  Dar es Salaam, wakikabiliwa na makosa kadhaa yakiwemo ya kushindwa kujisajili na kuwasilisha taarifa za shughuli wanazozifanya kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi [WCF].

Washtakiwa hao, Malakkara Semis na Shafeek M. Purayil ni Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni ya SPASH  INTENATIONAL CO. LTD. Silas Shemdoe na Deusdedit Samwel Kibassa ambao ni  Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni ya ENCC CONSULTANTS.

Wengine ni Wakurugenzi Watendaji wa LASAR LOGISTIC, Abshir Farah Gure na Farhiya Hersiwarsame, wakati Mshtakiwa mwingine ni Josephat Alexander ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KAMANDA SECURITY GUARDS CO. LTD.

 Washtakiwa wamesomewa mashtaka yao na waendesha mashtaka tofauti wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Emilly Kiria mbele ya Hakimu Mfawidhi Victoria Nongwa. Wanashtakiwa kinyume cha Kifungu  cha 71 (1) (a) na 71 (4) cha Sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi Sura ya 263 marejeo ya mwaka 2015.

Akisoma mashtaka yanayomkabili Joseph inadaiwa  Januari, mwaka 2018 walishindwa kujisajili na kutoa taarifa muhimu za shughuli zake na za wafanyakazi kwa Ofisa aliyeteuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF.

Ilidaiwa Januari 11, mwaka 2018 mshtakiwa huyo alishindwa kutoa taarifa mihimu za waajiriwa wake ikiwamo majina na mishahara ya wafanyakazi.

Katika kesi ya jinai namba 33 ya mwaka 2018, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Benson Mangowi  alidai washtakiwa  Malakhara Semis  na Shafeek Purayil  wa kampuni ya Spash International Co.Ltd  Desemba 25,mwaka 2017 walishindwa kusajili na kutoka taarifa muhimu za shughuli za kampuni kwa Mkurugenzi Mkuu wa WCF.

Pia walishindwa kutoa taarifa muhimu za wafanyakazi wao kwa Ofisa aliyeteuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF ambapo Septemba 6,mwaka 2017  washtakiwa hao walishindwa kutoa taarifa muhimu za wafanyakazi ikiwamo majina na mishahara.

Wakati kesi hiyo ikisomwa Malakhara hakuwapo mahakamani.

Katika kesi nyingine, wakili wa Serikali, Emma Msofe amedai washtakiwa Abshir Gure na Farhiya Warsame wa kampuni ya Lasar Logistic Limited, walishindwa kusajili na kupeleka taarifa muhimu kwa Mfuko wa WCF.

Alidai kuwa Oktoba 19,mwaka 2017 walishindwa kutoa taarifa muhimu zikiwamo majina na mishahara. Pia wanadaiwa Novemba 27,mwaka 2017 walishindwa kupelekwa taarifa za mfanyakazi wao, Lihikambo  Yunus ikiwamo kitambulisho cha Taifa, cha mpiga kura, leseni, mkataba wa ajira, taarifa za msharaha na taarifa ya polisi kwa afisa wa mfuko wa WCF.

Wakati kesi hiyo ikisomwa Abshir alikuwapo mahakamani lakini Farhiya hakuwapo.

Katika kesi namba 35,mwaka 2018, Wakili wa Serikali Mwandamizi Derrick Mukabatunzi alisisimama mahakamani hapo na Kuwaita washtakiwa Riziki Shemdoe na Deusdedit Kibassa ambapo wakili huyo aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa mmoja hakuweza kumpata na kwamba mwingine alikuwa akiuguliwa na mkewe Dodoma.

Hata hivyo, Mahakama imetoa hati za wito za Kuwataka mahakamani washtakiwa hao.

Washtakiwa wote wamekana mashtaka na upande wa mashtaka ulidai upelelezi umekamilika.

Hakimu Nongwa alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili ambapo kila mdhamini atasaini ahadi ya Sh 50 milioni, washtakiwa wote, wako nje kwa dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Februari 22,mwaka 2018 ambapo washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali (PH).

Akizungumza nje ya Mahakama Mwanasheria wa WCF, Deo Victor alisema kabla ya Mfuko  huo kuchukua hatua hii ya kuwafikisha  mahakamani, washtakiwa walipewa taarifa ya kutekeleza takwa hilo la kisheria katika tarehe mbalimbali, kati ya Septemba 2017 hadi Januari mwaka 2018 lakini walishindwa kutekeleza.
  Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni ya Spash International Co  Ltd  Shafeek Purayil (kulia) na Japhet Alexander  wa Kampuni ya Kamanda Security Guard Co. Ltd, wakipelekwa mahabusu ya Mahakama ya kisutu jijini Dar es Salaam leo Februari 19, 2018 baada ya kusomewa mashtaka mawili ya jinai kwa kushindwa kujisajili na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), na kuwasilisha taarifa za shughuli za Makampuni wanayoyaongoza kwa Mfuko huo. Washtakiwa wakipatikana na hatia wanakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka mitano (5), jela au faini isiyozidi shilingi milioni hamsini au vyote kwa pamoja.

Shafeek Purayil(mbele) na Japhet Alexander wakitoka mahakamani baada ya kusomewa mashtaka na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Bibi Victoria Nongwa.  
 Shafeek  Purayil
Meneja Matekelezo (Compliance Manager), wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Victor Luvena akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo. Alisema washtakiwa wengine Zaidi watapandishwa kizimbani Jumanne Februari 20, 2018 kwa makosa hayo hayo. Kulia ni Mwanasheria wa WCF, Bw. Deo Ngowi.
Meneja Matekelezo (Compliance Manager),  wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Victor Luvena akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo. Alisema washtakiwa wengine Zaidi watapandishwa kizimbani Jumanne Februari 20, 2018 kwa makosa hayo hayo.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.