Wednesday, August 21

JIACHIE: Maadhimisho Upandaji Miti Kitaifa kufanyika wilayani Kishapu

0


Na Robert Hokororo, Ofisi ya Mkurugenzi 

Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga inatarajia kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Upandaji Miti Kitaifa yatakayoanza Aprili 3,2018 hadi  Aprili 5,2018. 

Katika kilele cha maadhimisho hayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ambapo kauli mbiu ni ‘Tanzania ya Viwanda inawezekana, panda miti kwa maendeleo ya Viwanda’. 

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack wakati akizungumza ofisini kwake ambapo amebainisha kuwa madhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali. Miongoni mwa shughuli zinazotarajiwa kufanyika ni pamoja na zoezi la upandaji miti na kuwa kila kaya itakabidhiwa miche kwa ajili ya kuipanda katika maeneo yao na kutakiwa kuitunza. 

Mhe. Telack alisema kuwa lengo la zoezi hilo la upandaji wa miti ni kuifanya Wilaya ya Kishapu kuwa ya kijani kwa kuondoa hali ya jangwa inayoinyemelea. Sanjari na upandaji miti pia madhimisho hayo yataambatana na utoaji wa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wananchi ili kujenga uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Nyabaganga Taraba alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kutaja maeneo yatakayopandwa miti ni vijiji vya Mwatuju kata ya Shagigilu na Songwa. Alisema maadhimisho yataambatana pia na maonesho ya bidhaa za misitu pamoja na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali ambapo vyote hivyo vinatarajiwa kuoneshwa katika viwanja vya Shirecu. 

Mhe. Taraba alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kuendelea kupanda miti katika maeneo yao na kuitunza ili kuendelea kuhifadhi mazingira na kuepusha mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame. 

Tayari Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kishapu wameanza uhamasishaji na utoaji elimu ya uhifadhi wa misitu umeanza kufanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ikiwemo utoaji wa elimu kwa njia ya sinema.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.