Thursday, February 21

DC DAQARRO ATAKA WADAU WA ELIMU KUHAKIKISHA MPANGO WA LANES UNAENEA ARUSHA NA KULETA MATOKEO CHANYA

0
Mkuu wa wilaya ya Arusha Gabriel Daqarro amewataka waalimu na Afisa elimu kuhakikisha mpango wa KKK (LANES) unatiliwa mkazo sanjari na kuhakikisha wanafunzi wanajua kusoma kuandika na kuhesabu ili kuleta matokeo chanya na kufikia malengo ya serikali ya wananchi wote kujua kusoma. 


Akiongea wakati akifungua wiki ya kusoma na stadi za kukuza kusoma kuandika na kuhesabu (LANES) iliyofanyika katika Maktaba ya mkoa Dc Daqarro amesema kuwa wajibu huo ni wetu sote kuanzia nyumbani hadi mashuleni kuhakikisha kila moja wetu anatimiza wajibu wake. 


Amesema kuwa wiki kama hiyo ni ya kujitathmini tumefika wapi na tunaelekea wapi kama taifa kwa ajili ya kukuza uelewa wa vijana wetu kujua kuhesabu kusoma na kuandika ili kuwa na taifa linalopiga hatua kwa wananchi wake kujua kusoma. 


“Taifa limejipanga kuondoa wananchi wasio jua kusoma na kuandika ndio maana ilikaja na mkakati wa kkk hivyo kila mmoja wetu anawajibu kuhakikisha tunafikia malengo ya mkakati huu”alisema Daqarro
Kwa Upande wake Afisa elimu vielelezo Godfrey Augustino amesema kuwa wajibu wa wazazi ni kufuatilia maendeleo ya watoto wao na wao kama waalimu watahakikisha kila kijana anayepata nafasi anajua kusoma kuandika na kuhesabu lengo ni kuondoa vijana wanaomaliza elimu wakiwa hawajui kusoma na kuandika. 


Amesema kuwa hatavumilia kuona wilaya hiyo ikiwa ina vijana ambao hawajui kusoma wala kuandika na amejipanga kuhakikisha wanafikia malengo yalioanza kuonekana kwenye ufaulu kwa wilaya kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika ufaulu wa Darasa la saba mwaka huu. 


Awali mkutubi mkuu wa maktaba ya mkoa Rafiki Mvamba amesema kuwa analishukuru shirika Kwa kufadhili wiki hiyo na kuwataka watanzania kupenda kujisomea na kufuatilia watoto wao ili kujua kusoma na kuandika itakayopelekea taifa kuwa na wananchi wenye elimu ya kuweza kufikia malengo endelevu .


Amesema kuwa mpango huo LANES wa wiki ya kusoma ni kujitathmini na kuwafikia wanafunzi kujua uelewa wao katika kukuza stadi za kusoma kuandika na kuhesabu kuanzia watoto wa awali hadi vyuo vikuu kupenda kujisomea kwani elimu haina mwisho. 


“sisi kama maktaba tumejipanga kuhakikisha wanafunzi wote wanaofika hapa wanapata vitabu vyote wanavyohitaji sanjari na kuwapa nafasi na kuwaongoza pale wanapohitaji ili lengo ya kuwa na taifa lenye watu wanaojua kusoma na kuandika linafikiwa”alisema Mvamba

Share.

About Author

Leave A Reply