Tuesday, July 23

UGOMVI WA MALI WAMSUKUMA BILIONEA KUMKANA MTOTO WAKE

0


Si jambo la kawaida, baba anamkana mtoto wake wa kumzaa, na kutangaza kuwa hatahusika tena na mali zake.

Baba aliyetoa tangazo hilo kwenye magazeti nchini Tanzania ni Bw Ramanlal Patel, akimlenga mtoto wake Veer Patel.

Bwana Ramanlal ni mmoja wa wanahisa wakubwa wa Makampuni ya Motisun pamoja na mdogo wake Subhash Patel. Motisun ni moja ya makampuni makubwa na yenye mafaniko Tanzania na ni muunganiko wa makampuni 35. Familia ya Patel ni moja ya familia tajiri zaidi nchini Tanzania.

Katika tangazo ambalo limechapishwa kwenye magazeti Jumatano Mei 15, 2019, Bw Ramanlal Patel amesema Januari 31, 2019 alipata notisi ya kutolewa kwenye ukurugenzi wa makampuni hayo.

Kwenye notisi hiyo, Bw Ramanlal amedai kuwa, mtoto wake Veer Patel alipata kibali cha mahakama siku hiyo ya Januari 31 kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Huhimbili kufanyiwa uchunguzi wa akili, kwa mdai kuwa “mimi nina matatatizo ya akili na siwezi tena kufanya biashara…”taarifa ya Ramanlal imeeleza na kuongeza kuwa baada ya uchunguzi wa kina wa madaktari aligundulika hana tatizo lolote la akili na kupewa cheti cha daktari kuwa ana akili timamu.

“Hata hivyo, wakati nipo hospitali kwa siku hizo 17, nilitolewa kwenye nafasi yangu ya ukurugenzi wa makampuni ya Motisun na nafasi hiyo kuchukuliwa na Veer Patel …. kutokana na hayo yote, ninapenda kuufahamisha Umma kwamba kuanzia sasa Veer Ramanlal Patel si mtoto wangu tena wala msimamizi au mdhamini wangu na hahusiki na hatahusika na mali zangu zote na maisha yangu, nikiwa hai au nitapokuwa nimekufa…” sehemu ya taarifa ya Bw Ramanlal imesema.

Pia mfanyabiashara huyo ameutaarifu Umma kuwa hatawajibika kwa namna yeyotena wakopeshaji, mabenki, wauzaji na wasambazaji wote wanaofanya biashara na makampuni ya Motisun.

Gazeti la The Citizen limemnukuu msemaji wa makampuni ya Motisun Abubakar Mlawa ambaye amesema kuwa mchakato wa kuondolewa kwa Bw Ramanlal kwenye bodi ya wakurugenzi wa makampuni hayo haukufanyika na mtu mmoja.

Pia amesema kuwa kwa zaidi ya miaka 10 Bw Ramanlal amekuwa na matatizo ya kiafya hali iliyomfanya kutokuwa kazini kwa muda mrefu hali iliyopelekea bodi kumchagua mtoto wake pekee wa kiume kuchukua nafasi ya baba yake.

Hata hivyo amesema, Ramanlal ataendelea kumiliki hisa zake na ataendelea kupokea gawio la faida kutokana na hisa zake.

Kwa mujibu wa tovuti ya makampuni ya Motisun, Veer Patel, ndiye Afisa Mtendaji mdogo zaidi katika makampuni hayo na anasimamia biashara ya huduma za hoteli za kampuni hiyo. Pia ana shahada ya uzamili kwenye masoko aliyoipata nchii Uingereza.

Motisun wanamiliki hoteli maarufu nchini Tanzania za White Sands na Sea Cliff.

Kampuni hiyo pia ndiyo wazalishaji wa juisi na maji chapa ya Sayona, saruji chapa Mamba. Bidhaa nyingine maarufu ni rangi, mabati na matangi ya kuhifadhia maji ya chapa Kiboko.

Kampuni hiyo pia inamtandao wa biashara nchini Msumbiji, Zambia na Uganda.

Share.

About Author

Leave A Reply